Ujumbe wa AU wawasili Burundi baada ya kuondoka Ban Ki-Moon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1927-ujumbe_wa_au_wawasili_burundi_baada_ya_kuondoka_ban_ki_moon
Rais Macky Sall wa Senegal anaongoza ujumbe wa marais wanne wa Umoja wa Afrika ambao umewasili nchini Burundi leo Alkhamisi kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo tangu mwezi Aprili mwaka jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2016 11:59 UTC
  • Ujumbe wa AU wawasili Burundi baada ya kuondoka Ban Ki-Moon

Rais Macky Sall wa Senegal anaongoza ujumbe wa marais wanne wa Umoja wa Afrika ambao umewasili nchini Burundi leo Alkhamisi kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo tangu mwezi Aprili mwaka jana.

Marais wengine waliomo kwenye ujumbe huo ni Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Muhammed Ould Abdul Aziz wa Mauritania, Ali Bongo wa Gabon na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn. Ujumbe huo unatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na shakhsia muhimu wa nchi hiyo wakiwemo viongozi wa serikali na wale wa upande wa upinzani. Safari ya ujumbe huo wa Umoja wa Afrika inafanyika siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuitembelea nchi hiyo na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza mjini Bujumbura. Kwa mujibu wa Ban, Rais Nkurunziza ameunga mkono juhudi za kufanyika mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo huo wa kisiasa. Hata hivyo, muungano wa vyama vya upinzani nchini humo CNARED ambao aghalabu ya viongozi wake wako nje ya nchi, umepinga mpango wa kufanyika mazungumzo hayo. Mwenyekiti wa muungano huo Leonard Nyangoma amemtaja Rais Nkurunziza kama kiongozi kigeugeu ambaye hana nia ya dhati ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo. Imeripotiwa kuwa, zaidi ya watu 400 wameuawa huku wengine zaidi ya laki 2 wakilazimika kuyakimbia makazi yao, kutokana na kushadidi wimbi la mchafukoge nchini Burundi tangu Aprili mwaka jana 2015, baada ya Nkurunziza kutangaza azma yake ya kuwania urais kwa muhula wa tatu.