Feb 26, 2016 16:16 UTC
  • UN: Kuna ushahidi wa jinai za kivita Libya

Umoja wa Mataifa umesema wahusika wote katika mgogoro wa Libya wametenda jina za kivita pamoja na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti ya maafisa sita wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, kuna ushahidi wa kuuawa mateka, kuuawa wanaharakati maarufu wa kike, utesaji, jinai za kingono, utekaji nyara, hujuma za kiholela za jeshi katika maeneo ya raia na kudhalilishwa watoto nchini Libya kati ya mwaka 2014 na 2015.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein amesema katika taarifa kuwa, watu wanaofungamana na serikali na wasiofungamana na serikali wamekiuka haki za binadamu na kutekeleza vitendo ambavyo vinahesabiwa kuwa ni jinai za kivita.

Katika ripoti ya kurasa 95 iliyochapishwa Alhamisi, maafisa wa Umoja wa Mataifa wamewahoji mashuhuda na waathirika 200, mbali na kurekodi malalamiko 900.

Libya ilitumbukia katika ghasia na machafuko ya ndani baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Muammar Gaddafi mwaka 2011. Maeneo kadhaa ya nchi hiyo kwa sasa yanadhibitiwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Hadi sasa serikali ya umoja wa kitaifa haijaundwa nchini humo kutokana na mivutano iliyopo kati ya makundi tofauti ya kisiasa.

Tags