Nov 25, 2016 05:59 UTC
  • Kikao cha nne cha viongozi wa Kiarabu na Kiafrika na changamoto zake

Kikao cha nne cha pamoja baina ya viongozi wa Kiarabu na Kiafrika kimefanyika katika anga ya kushadidi tofauti na mivutano ya kisiasa baina ya pande mbili.

Lengo la kikao hicho kilichosimamiwa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu na Kamishna wa Umoja wa Afrika, ni kuanzishwa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya pande mbili, kuanzishwa maeneo ya kiuchumi ya pamoja kati ya Afrika na nchi za Kiarabu, kuchunguza mapendekezo yaliyotolewa katika kikao kilichopita na ambacho kilifanyika nchini Kuwait, kuboresha uhusiano wa nchi wanachama na kadhalika kuanzishwa kamisheni maalumu yenye lengo la kuunga mkono wafanyakazi wahamiaji. Katika kikao hicho cha pamoja, kilichohudhuriwa na viongozi wa nchi za Kiafrika na wawakilishi wa mawaziri wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiafrika kwa kushirikiana na mashirika na asasi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, kuliibuka maamuzi ya ghafla ya nchi nne za Morocco, Saudia, Imarati na Bahrain ya kutaka kujiondoa kikaoni hali iliyobadilisha anga ya mkutano huo.

Viongozi wa Kiarabu na Kiafrika wakielekea kwenye mkutano

Hii ni katika hali ambayo kufanyika kikao hicho kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa nchi nyingi za eneo la Mashariki ya Kati hasa kwa kuzingatia anga ya kisiasa na tofauti za ndani, matatizo ya kiuchumi na migogoro ya kijamii ya nchi hizo za Kiarabu na Kiafrika. Ilitegemewa kuwa, kwa kuvutia uhusiano wa nchi washiriki, ingewezekana kutatuliwa baadhi ya matatizo hayo. Hata hivyo kutoshiriki kwa nchi zilizotajwa, kumesababisha ukwamishaji wa malengo yaliyokusudiwa. Hata kama sababu kuu iliyoifanya Morocco kujiengua katika mkutano huo inatajwa kuwa ni mpango wa kutaka kuongezewa uwezo wa kisiasa wa Harakati ya Polisario, huku Saudia na Bahrain nazo zikijiondoa kutokana na ushirikiano wao na Morocco. Lakini kile kinachoonekana ni kwamba, kuongezewa mamlaka ya kisiasa nchi ya Kuwait katika suala zima la kutoa maamuzi ya kisiasa na kiuchumi, ndio sababu kuu iliyozifanya nchi hizo za Kiarabu hususan Saudia  kujiengua kutoka kwenye mkutano.

Wasichana wa Kiafrika wanaofanya kazi nchi za Kiarabu wakiandamana

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Kuwait imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kupanua ustawi wake wa kisiasa na kiuchumi kati yake na nchi za Kiafrika, katika hali ambayo Saudia nayo kutokana na kufeli siasa zake katika eneo la Mashariki ya Kati, imeelekeza satwa yake katika nchi hizo za bara la Afrika.

Mbali na Saudia kukabiliwa na matatizo ya nje, kadhalika inakabiliwa na matatizo na changamoto za ndani, kubwa zaidi ikiwa ni mgogoro wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kwa miaka kadhaa sasa Saudia imekuwa ikipanua wigo wake katika nchi za bara la Afrika. Uungaji mkono wa muda mrefu wa Riyadh kwa makundi ya kigaidi na wapinzani wa nchi za Kiafrika, kutuma masheikh wa Kiwahabi kwa lengo la kueneza fikra za kundi hilo, na kuwekeza katika sekta tofauti za kiuchumi za nchi hizo, ni miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Saudia katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa muktadha huo hivi sasa inaonekana kuwa, kudhihiri uwezo wa Kuwait katika kikao hicho ni suala ambalo halikuifurahisha Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu. Hii ni kusema kuwa, kuchukua hatua mpya katika utekelezaji wa siasa zake mpya, serikali ya Kuwaita imeweza kutangaza ufunguzi wa sanduku la mikopo kwa ajili ya nchi za Afrika.

Sehemu ya unyanyasaji dhidi ya wafanyakazi wa Kiafrika ndani ya nchi za Kiarabu

Hata hivyo nchi za Kiafrika zinazoshiriki kikao hicho zina malengo mengine mbalimbali. Akthari ya nchi hizo zinashiriki mkutano huo kwa lengo la kuboresha uchumi wao, kuomba msaada kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi, kuvutia uwekezaji kwa ajili ya kutatua matatizo ya kiuchumi kama vile ukosefu wa ajira, na pia kukabiliana na matatizo ya kisiasa ya ndani.

Aidha raia wengi wa mataifa hayo ya Kiafrika wanafanya kazi katika nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi katika mazingira magumu huku wakilipwa kiasi kidogo sana cha mshahara. Kwa kuzingatia hali hiyo, ilitazamiwa kikao hicho kiwe sababu ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa. Hata hivyo kinyume chake kimekumbwa na mkwamo kutokana na kupenda makuu kwa baadhi ya nchi za Kiarabu, suala ambalo limeuweka uhusiano wa nchi za Kiarabu na Kiafrika katika hali na hatima isiyojulikana.

 

Tags