Maelfu waandamana Burundi wakiupinga Umoja wa Mataifa na Ubelgiji
Maelfu ya wananchi wa Burundi wameandamana katika mji mkuu Bujumbura wakiupinga Umoja wa Mataifa pamoja na siasa za Ubelgiji za kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.
Wananchi hao wameandamana wakipinga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kuwatangaza wajumbe wa kamisheni ya uchunguzi kuhusiana na kile kilichoelezwa kuwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi.
Maandamano hayo yanakuja siku moja tu baada ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuunda kamati huru ya kuchunguza ripoti za kuweko vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi. Kamati hiyo inaundwa na Jaji Fatsah Ouguergouz raia wa Algeria ambaye ni ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, wakili Reina Gansu wa Benin na Francosi Hampson wa Uingereza ambaye ni Profesa katika masuala ya sheria.
Baadhi ya waandamanaji aidha walikusanyika mbele ya ubalozi wa Ubelgiji mjini Bujumbura wakilalamikia uingiliaji wa nchi hiyo ya Ulaya katika masuala ya ndani ya Burundi.
Waandamanaji hao wametangaza kuwa, Ubelgiji ina mkono katika mgogoro wa nchi hiyo.
Burundi imekuwa ikishuhudia hali ya mchafukoge tangu mwezi Aprili mwaka jana, baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea kwa muhula wa tatu katika uchaguzi wa rais uliopita.
Kwa mujibu wa asasi za kutetea haki za binaadamu nchini Burundi, hadi sasa kwa akali watu 450 wamekwishapoteza maisha kufuatia machafuko hayo, huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.