Mgombea wa upinzani ashinda kiti cha Urais Gambia
Adama Barrow, mgombea wa muungano wa upinzani nchini Gambia amembwaga Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh katika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo ambao matokeo yake hayakutarajiwa.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Gambia, Barrow ameshinda uchaguzi wa Rais kwa kupata asilimia 45 na nusu ya kura huku Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 22 akiambulia asilimia karibu 37 ya kura. Watu 890,000 kati ya jamii ya Gambia ya watu milioni mbili walishiriki katika uchaguzi huo uliowajumuisha wagombea watatu wa kiti cha urais. Wagombea hao ni Rais Yahya Jammeh wa Gambia anayeondoka madarakani, Adama Barrow, aliyeviwakilisha vyama saba vya upinzani na Mammah Kandeh, mwanachama wa zamani wa chama tawala ambaye alikiwakilisha chama kimoja kilichoundwa hivi karibuni cha Gambia Democratic Congress.
Yahya Jammeh amekubali kushindwa katika uchaguzi wa Rais wa majuzi baada ya kushika hatamu za uongozi kwa miaka 22, katika hali ambayo ilitabiriwa kuwa iwapo mara hii angeshinda tena na kama pasingefikiwa makubaliano, basi mgogoro wa kisiasa na mivutano ingeshtadi huko Gambia. Rais wa Gambia alisisitiza kabla ya matokeo haya kwamba, hatokubali matokeo yoyote yatakayomuonyesha kuwa ameshindwa katika kinyang'anyiro hicho cha urais. Wakazi wa mji mkuu Banjul walimiminika katika mitaa mbalimbali ya mji huo mkuu kusherehekea ushindi wa Adama Barrow, mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi, licha ya kuwepo askari usalama. Uchaguzi wa Rais umefanyika huko Gambia ambapo mivutano ya kisiasa ilikuwa imeshtadi nchini humo khususan katika wiki za hivi karibuni. Yahya Jammeh ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1994 akiwa katika kampeni za uchaguzi hivi karibuni alitishia kuviua vyama vya upinzani. Jammeh pia alitoa radiamali kwa ripoti zilizotolewa na wanaharakati wa haki za binadamu na kuwataja wanaharakati hao kuwa ni mapepo wabaya. Wanaharakati hao wa haki za binadamu siku kadhaa zilizopita walitoa ripoti ambayo ilikosoa vikali hali ya mambo huko Gambia na kulaani pia unyongaji na ukamataji watu kiholela unaofanywa na wanamgambo, idara za kiintelijinsia na usalama za nchi hiyo. Watetezi hao wa haki za binadamu walisema katika ripoti yao hiyo waliyoitoa kwa mnasaba wa kufanyika uchaguzi huu wa rais wa majuzi huko Gambia kuwa, hali ya hofu na vitisho wanavyofanyiwa shakhsia wa kisiasa wa mrengo wa upinzani na wanaharakati huko Gambia inaondoa uwezekano wa kukosolewa kwa namna yoyote Rais Yahya Jammeh na serikali yake. Hii ni mara ya kwanza nchini Gambia ambapo vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani vimeweza kuweka kando hitilafu zao za kivyama na kuzingatia tu maslahi ya taifa ya watu wa nchi hiyo. Katika nchi nyingi za bara la Afrika viongozi wamekuwa wakitumia nguvu za kijeshi, ukandamizaji na vitisho kwa lengo la kuendelea kubaki madarakani, lakini kulegeza kamba Yahya Jammeh mara hii tunaweza kusema kuwa kumetokana na mtawala huyo kutambua hali halisi ya nchi yake na kuafiki pamoja na kuheshimu matakwa ya wananchi ya kuhitaji mabadiliko. Wale wanaoikosoa serikali wanaamini kuwa, wananchi wa Gambia walikuwa wamechoshwa na utawala wa miaka 22 wa Rais Jammeh na sasa wanahitaji mabadiliko na hatua mpya za kisiasa nchini mwao.
Kwa msingi huo Rais mteule anakabiliwa na safari ndefu mbele yake kutokana na kuongezeka matatizo ya kiuchumi, umaskini, kukosekana uhuru wa mtu binafsi na wa kiraia na kukandamizwa wapinzani; mambo ambayo yamekuwa yakiifanya serikali ya Yahya Jammeh ikosolewe.