Mkapa yuko Burundi kwa ajili ya kuhuisha mazungumzo ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21019-mkapa_yuko_burundi_kwa_ajili_ya_kuhuisha_mazungumzo_ya_amani
Benjamin Mkapa mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa Burundi yuko mjini Bujumbura kwa shabaha ya kuhuisha mazungumzo ya amani ya nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 08, 2016 09:59 UTC
  • Mkapa yuko Burundi kwa ajili ya kuhuisha mazungumzo ya amani

Benjamin Mkapa mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa Burundi yuko mjini Bujumbura kwa shabaha ya kuhuisha mazungumzo ya amani ya nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa.

Mkapa ambaye ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwasili jana mjini Bujumbura kwa mwaliko wa Rais Pierre Nkurunziza, lengo likiwa ni kuhuisha mazungumzo ya amani yaliyokwama kati ya serikali ya nchi hiyo na wapinzani.

Mpatanishi huyo wa mgogoro wa Burundi leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Nkurunziza wa wa nchi hiyo. Taarifa zaidi zinasema kuwa, katika safari yake hiyo ya siku tatu nchini Burundi na katika mazungumzo yake Rais Nkurunziza na mrengo wa upinzani, Benjamin Mkapa anatarajiwa kuelezea mipango yake mipya ya utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo hadi kufikia katikati ya mwaka ujao.

Benjamin Mkapa akiwasili Burundi

Aidha mpatanishi huo wa mgogoro wa Burundi anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa dini na wawakilishi wa jumuiya za kiraia na za kimataifa katika nchi hiyo.

Burundi imekuwa ikishuhudia hali ya mchafukoge tangu mwezi Aprili mwaka jana, baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa rais uliopita ambao ulitawaliwa na malalamiko mengi.

Kwa mujibu wa asasi za kutetea haki za binaadamu nchini Burundi, hadi sasa zaidi ya watu 400 wamekwishapoteza maisha kufuatia machafuko hayo, huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.