Mufti wa Algeria aikosoa vikali Saudia kwa kuongeza gharama za Hija, Umrah
Mufti Mkuu wa Algeria ameukosoa vikali utawala wa Saudia Arabia kwa vitendo vyake vya kuwazuia Waislamu kutekekeleza ibada ya faradhi ya Hija na pia Umrah
Mufti Sheikh Muhammad Ali Ferkous amesema katika mahojiano na tovuti ya Islam Al Youm kwamba: "Watawala wa Saudia wanatumia ibada ya Hija kujitajirisha na hivi sasa wao ni misdaki na kielelezo cha wazi ya 'sad an Sabilillah' kwa maana ya watu wanaowazuia waja katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wanawazuia Waislamu kutekeleza Hija na Umrah."
Sheikh Ali Ferkous ameendelea kukosoa utendaji wa watawala wa Saudia katika ibada ya Hija na kusema kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za Hija na Umrah ni jambo ambalo limewashangaza Waislamu na kupelekea wapoteze matumaini.
Mufti Mkuu wa Algeria ameongeza kuwa Saudia inaitazama Hija na Umra kama njia ya kujitajirisha na kufanya biashara.
Sheikh Ali Ferkous amemtaka mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia kuchukua hatua za kuzuia utekelezwaji wa mpango huo wa kuongeza kwa asilimia kubwa gharama za Mahujaji na wanaoenda Umrah.
Hivi karibuni wakuu wa Saudia walitangaza uamuzi wao wa kuongeza gharama za Waalgeria wanaoenda Hija au Umra kwa asilimia 35. Nchi kadhaa kama vile Misri, Uturuki, Morocco na Jordan zimekosoa vikali hatua ya Saudia kuongeza gharama za Visa.
Katika mpango huo wa kuongeza malipo ya Visa Saudia imependekeza visa ya kuingia katika ufalme huo mara moja kuwa dola 533, ikiwa ni nyongeza kubwa ikilinganishwa na malipo ya zamani ya dola 93. Aidha visa ya miezi sita sasa itagharimu dola $800 na ya mwaka mmoja dola $1333. Saudia inakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na ongezeko la gharama za hujuma yake dhidi ya nchi jirani ya Yemen na pia kushuka bei ya mafuta duniani na hivyo inajaribu kufidia pengo hilo kwa kuwatoza kiasi kikubwa cha fedha mamilioni ya Waislamu wanaoenda nchini humo kwa ajili ya ibada katika miji mitakatifu ya Makka na Madina.