AU yaitaka Sudan Kusini ipambane na ukatili dhidi ya wanawake
Umoja wa Afrika umeitaka serikali ya Sudan Kusini ichukue hatua madhubuti za kupambana na ukatili dhidi ya wanawake nchini humo.
Mjumbe Maalumu wa Kamisheni ya Amani, Usalama na Wanawake ya Umoja wa Afrika, Bineta Diop alifanya ziara nchini Sudan Kusini ambapo alisema kuwa, wanawake nchini humo ni wahanga wa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia na kwamba ukosefu wa amani unashuhudiwa katika maeneo yote ya nchi hiyo.
Bineta Diop amesema kuwa iwapo kutakuwepo na azma ya kisiasa kwa ajili ya kuwafikisha wahusika wa jinai hizo dhidi ya wanawake kwenye vyombo vya sheria, basi tabaka hilo la jamii linaweza kuwa na matarajio ya mustakbali mwema.
Mjumbe Maalumu wa Kamisheni ya Amani, Usalama na Wanawake ya Umoja wa Afrika pia amebainisha kuwa, umoja huo utafanya juhudi za kuhakikisha kuwa wanawake wanapata haki zao na wahanga wa ukatili huo wanarejeshewa heshima ya binadamu.
Tangu mwaka 2013 Sudan Kusini ilikumbwa na mzozo wa ndani na mgogoro wa kisiasa vilivyosababishwa na mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na makamu wake wa zamani Riek Machar ambaye ni kiongozi wa waasi wa nchi hiyo.