Uwezekano wa Jammeh kuondolewa kwenye kiti cha urais kwa nguvu za kijeshi
Rais wa Senegal amesema kuna uwezekano rais wa Gambia kuondolewa kwa nguvu za jeshi katika kiti cha urais baada ya kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi.
Macky Sall rais wa Senegal akizungumza Ijumaa amesema chaguo la mwisho la mgogoro wa kisiasa Gambia ni kutumia nguvu za majeshi ya kimataifa kumlazimisha Yahya Jammeh akubali kushindwa katika uchaguzi.
Sall amesema Senegal ina matumaini kuwa mazungumzo ya kisiasa na onyo alilopewa Jammeh kuhusu hatima yake hasa kushtakiwa katika mahakama za kimataifa ni jambo ambalo litamshawishi rais huyo wa Gambia abadilishe uamuzi wake wa kukataa matokeo ya uchaguzi.
Tahadhari hiyo ya rais wa Senegal imekuja siku chache baada ya viongozi kadhaa wa nchi za Afrika Magharibi kujaribu kumshawishi Jammeh aondoke madakrani lakini jitihada hizo hazijazaa matunda.
Siku chache zilizopita, Jammeh aliwashangaza na kuwaacha vinywa wazi Wagambia na duru za kisiasa barani Afrika alipoyakataa katakata matokeo ya uchaguzi, kama alivyopongezwa na kila mtu alipojitokeza hadharani siku ya tarehe Pili Desemba kumpongeza Adama Barrow, mgombea urais kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani hata kabla hajatangazwa mshindi rasmi wa kinyang'anyiro hicho.
Rais Jammeh aliyakataa matokeo ya uchaguzi wa rais kwa madai ya kile alichokiita makosa yasiyokubalika yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gambia na kutaka uitishwe uchaguzi mwingine mpya.