Wapinzani wazidi kutiwa mbaroni Burundi, wasiwasi waongezeka nchini
Mkuu wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Burundi (Iteka) amesema anatiwa wasiwasi na kuzidi kutiwa mbaroni wapinzani nchini humo.
Ansachaire Nikoyagize amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, ana wasiwasi na kuendelea kutiwa nguvuni wapinzani nchini humo na kusisitiza kuwa, viongozi wa nchi hiyo wamesababisha anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuwa ya hofu na machafuko. Anschaire Nikoyagize ameongeza kuwa, vitendo vya bughdha na mateso ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wapinzani na askari usalama tangu miezi mitatu iliyopita vimeongezeka sana. Mkuu wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu ya nchini Burundi (Iteka) amesema, jumuiya hiyo imethibitisha kutiwa mbaroni wapinzani 272 mwezi Oktoba huku wengine 16 wakiwa hawajulikani walipo. Amesema watu wengine 541 walitiwa mbaroni na wengine 55 walitoweka katika wiki mbili za kwanza za mwezi huu wa Disemba.
Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwaka jana kufuatia hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Wapinzani kwa upande wao waliitaja hatua hiyo ya Nkurunziza kuwa ni kinyume na katiba na kumtuhumu kuwa amepuuza makubaliano ya amani ya Burundi yaliyohitimisha vita vya ndani nchini humo.