Polisi: Waziri auawa kwa kufyatuliwa risasi Bujumbura, Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22549-polisi_waziri_auawa_kwa_kufyatuliwa_risasi_bujumbura_burundi
Waziri wa Mazingira wa Burundi ameuawa kwa kufyatuliwa risasi na mtu asiyejulikana usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu Bujumbura.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 01, 2017 03:49 UTC
  • Polisi: Waziri auawa kwa kufyatuliwa risasi Bujumbura, Burundi

Waziri wa Mazingira wa Burundi ameuawa kwa kufyatuliwa risasi na mtu asiyejulikana usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu Bujumbura.

Pierre Nkurikiye, msemaji wa polisi ya Burundi amesema Emmanuel Niyonkuru, Waziri wa Mazingira, Maji na Mipango wa nchi hiyo ameuawa saa sita na dakika 45 hivi usiku wa kuamkia leo, alipokuwa akielekea nyumbani kwake Rohero, viungani mwa mji mkuu.

Polisi ya Burundi imeongeza kuwa, mwanamke mmoja anayusishwa na mauaji hayo ya waziri amekamatwa huku polisi ikianzisha msako wa kuwatafuta wahusika na kubaini lengo lao la kutekeleza ukatili huo.

Marehemu Hafsa Mossi, waziri wa zamani wa Burundi

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na marafiki wa waziri huyo aliyeuawa.

Mauaji haya yanajiri miezi michache baada ya waziri wa zamani na mwakilishi wa Burundi katika Bunge la Afrika Mashariki EALA, Hafsa Mossi kuuawa karibu na nyumba yake mjini Bujumbura kwa kufyatuliwa risasi mbili na watu wasiojulikana. Mossi ambaye pia alikuwa mwandishi wa habari mtajika, aliuawa Julai 13 baada ya kushuka kwenye gari lake kwenda kutizama gari lenye vioo vyeusi lililokuwa limegonga gari lake kutoka nyuma.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Burundi katika miezi kadhaa iliyopita imeshuhudia utulivu wa kiasi fulani, baada ya kukabiliwa na taharuki na machafuko yaliyotokana na hatua ya Rais Nkurunziza kuwania tena urais kwa muhula wa tatu mwaka 2015.