Jan 02, 2017 07:06 UTC
  • Ahadi ya Rais wa Nigeria ya kurejesha amani na usalama wa nchi

Katika hali ambayo, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema katika ujumbe wake kwa mnasaba wa mwaka mpya wa 2017 kwamba, ameazimia kuchukua hatua za kurejesha usalama na uthabiti wa nchi hiyo na wa kieneo, kwa mara nyingine tena kundi la kigaidi la Boko Haram limetishia kutekeleza operesheni za kigaidi katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Katika ujumbe wake huo wa mwaka mpya, Rais Buhari amewaita katika meza ya mazungumzo waasi wa Niger Delta na kubainisha kwamba, serikali yake inafanya mikakati ya kupatikana amani ya kudumu baina yake na waasi hao katika mwaka huu wa 2017.

Rais Buhari ameashiria wasiwasi wa kiusalama wa nchi yake, likiwemo tishio la kundi la kigaidi la Boko Haram na kusema kuwa: Ninataka kuwahakikishia wananchi wa Nigeria kwamba, katika mwaka huu mpya vikosi vyetu vya usalama na vya kiulinzi vimejiandaa kuliko wakati mwingine wowote kwa ajili ya kutekeleza nafasi yao ya kisheria katika kulinda roho na mali za wananchi.

Waasi wa Niger Delta

Ahadi hiyo ya Rais Buhari inatolewa katika hali ambayo, mashambulio ya waasi wa Niger Delta dhidi ya taasisi za mafuta za Nigeria yaliyokwenda sambamba na kupungua bei ya mafuta katika soko la dunia, yamepelekea kuzorota uchumi wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika inayofahamika kama ngome kubwa zaidi ya uchumi wa Afrika. Mwaka uliopita, waasi wa Niger Delta walifanya mashambulio makubwa dhidi ya taasisi za mafuta za Nigeria na mashirika ya mafuta ya kigeni katika eneo hilo. Waasi hao wanataka wapatiwe hisa zaidi ya utajiri wa Nigeria katika sekta ya nishati.

Hivi karibuni Rais wa Nigeria alitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuwatimua wanamgambo wa Boko Haram kutoka katika ngome yao kubwa kwenye msitu wa Sambisa na kwamba, kwa sasa wanachama wa kundi hilo hawana tena mahala pa kujificha.

Abubakar Shekau, Kiongozi wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Hata hivyo Abubakar Shekau, kiongozi wa Boko Haram ametoa mkanda wa video ambapo mbali na kueleza kwamba, madai ya serikali ya Rais Buhari ya kusambaratika kundi lao hayana msingi wowote, amewataka wapiganaji wake kushadidisha operesheni za kijeshi dhidi ya raia na vikosi vya serikali.

Hivi sasa lililo wazi ni kwamba, licha ya juhudi za serikali ya Nigeria za kupambana na Boko Haram, lakini inaonekana kuwa, harakati za kigaidi za kundi hilo zingali zinaendelea kushuhudiwa nchini humo na katika maeneo ya nchi jirani.

Operesheni za kijeshi za Boko Haram za miaka saba zimevuka mpaka wa nchi hiyo na kuingia katika maeneo ya nchi jirani ambapo inakadiriwa kwamba, watu 20,000 wamekwishauliwa hadi sasa, tangu kundi hilo lianzishe mauaji na operesheni zake. Aidha raia wengi wa Nigeria hasa wa maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo wamelazimika kuyakimbia makazi ya yao kutokana na operesheni za mauaji ya Boko Haram. Raia hao ambao wamekimbilia katika maeneo mengine na kuomba hifadhi huko, wanakabiliwa na matatizo mengi hasa ya uhaba wa chakula na dawa.

Wanajeshi wa Nigeria katika msitu wa Sambisa

Hivi sasa licha ya Rais Buhari kwa mara nyingine tena kuzungumzia suala la kulitokomeza kundi la Boko Haram, kufanyika mazungumzo na waasi wa Niger Delta na kutilia mkazo juu ya kurejesha amani na uthabiti wa Nigeria, lakini inavyoonekana ni kuwa, lengo hilo litafikiwa tu, pale viongozi wa nchi hiyo watakapokuwa tayari kubadilisha utendaji wao katika fremu ya kupunguza mivutano na wakati huo huo, watazame upya siasa zao zilizokwenda kombo za huko nyuma na kupiga hatua moja mbele kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano wa ndani baina ya raia wa nchi hiyo.

Kushadidi mashinikizo dhidi ya jamii ya Waislamu wa Nigeria katika mwaka uliomalizika wa 2016, ni jambo linalotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, limechochea zaidi moto wa mivutano na hitilafu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye bado anashikiliwa kizuizini

Filihali, Waislamu wa Nigeria wanasubiri kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambapo licha ya kutolewa amri ya mahakama ya kuachiliwa huru mwanazuoni huyo, hadi sasa takwa hilo bado halijatekelezwa.

Kwa mukatadha huo, inaonekana kuwa, viongozi wa Nigeria watafanikiwa kurejesha amani na uthabiti na kufanikiwa katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram pale tu watakapoweza kuyapatia mwarubaini matatizo ya ndani sanjari na kuleta umoja na mshikamano baina ya raia na wakati huo huo kuupiga jeki zaidi ushirikiano wa kieneo katika vita dhidi ya ugaidi.

Tags