Taasisi ya haki za binaadamu nchini Burundi yapigwa marufuku na serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i22765-taasisi_ya_haki_za_binaadamu_nchini_burundi_yapigwa_marufuku_na_serikali
Taasisi ya miaka mingi iliyokuwa ikiendesha shughuli za kibinaadamu nchini Burundi imepigwa marufuku na serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2017 13:48 UTC
  • Taasisi ya haki za binaadamu nchini Burundi yapigwa marufuku na serikali

Taasisi ya miaka mingi iliyokuwa ikiendesha shughuli za kibinaadamu nchini Burundi imepigwa marufuku na serikali.

Viongozi wa serikali ya Burundi wametangaza Jumanne ya leo kwamba, taasisi hiyo ya zamani iliyokuwa ikijishughulisha na kuchunguza uvunjwaji wa haki za binaadamu katika kipindi cha miaka miwili ya mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo, sasa haitaendelea tena na shughuli zake hizo. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Burundi imesema kuwa, taasisi hiyo maarufu kwa jina la Iteka imekuwa ikiendesha harakati zake kwa namna isiyo sahihi na kwamba shughuli zake zimechochea chuki na kuibua hali ya mpasuko katika jamii ya Warundi.

Mauaji nchini Burundi

Hii ni katika hali ambayo taasisi hiyo ya Iteka imesema kuwa, hatua hiyo ya serikali ya Bujumbura haikuishangaza kwa kuwa, hivi sasa viongozi wa serikali ya nchi hiyo wanafanya kila wawezalo kuzuia kuakisiwa uvunjwaji wa haki za binaadamu ndani ya taifa hilo. Inafaa kukumbusha kwamba taasisi hiyo ya haki za binaadamu nchini Burundi Iteka, iliasisiwa mwaka 1991. Burundi ilitumbukia katika hali ya mchafukoge tangu mwezi April mwaka jana, kufuatia hatua ya chama tawala cha nchi hiyo CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea kwa muhula wa tatu katika uchaguzi wa rais uliopita, hatua ambayo ilitajwa na wapinzani kuwa ni kinyume cha katiba.