Jan 07, 2017 15:55 UTC
  • Wanajeshi wazidi kuhatarisha hali ya mji wa Abidjan, Ivory Coast

Hali ya taharuki imeendelea kutanda katika mji mkubwa wa kibiashara wa Abidjan nchini Kodiva kufuatia askari wanaopinga kiwango kidogo cha mshahara kufyatua risasi ovyo mjini humo.

Habari zinasema kuwa, leo Jumamosi ikiwa ni siku ya pili tangu askari hao waanzishe wimbi la malalamiko yao ya kudai nyongeza ya mishahara, wameendelea kufyatua ovyo risasi katika kambi  moja ya kijeshi ya mji huo.

Wakati huo huo wakazi wa mji wa Bouaké, wameviambia vyombo vya habari kwamba leo Jumamosi kumesikika milio ya risasi na hivyo kuwazidishia wasi wasi.

Itafahamika kuwa, Ijumaa ya jana askari ambao kwa sasa wanaudhibiti mji wa Bouaké walianzisha wimbi la malalamiko ya kudai nyongeza ya mshahara na walifyatua risasi ovyo. Kwa mujibu wa habari hiyo, askari hao wenye hasira wamefunga lango la kuingilia mji huo unaokadiriwa kuwa na wakazi karibu nusu milioni nchini Ivory Coast.

Askari wanaodaiwa kufanya machafuko Kodivaa

Wakati huo huo, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo imetangaza azma yake ya kusikiliza malalamiko ya askari hao. Mwaka 2014 kulizuka mgogoro wa kisiasa na kijeshi sawa na huo ambao ulitokana na matatizo ya kiuchumi na kupelekea askari kupigania nyongeza ya mishahara yao.

Tags