Kurejea utulivu Côte d’Ivoire na ahadi za Rais Alassane Ouattara
Hatimaye utulivu umerejea kwa kiasi fulani nchini Côte d’Ivoire kufuatia mgogoro wa kisiasa na kiusalama wa siku kadhaa baada ya rais wa nchi hiyo kukubali matakwa ya askari waasi na kuachiliwa huru Waziri wa Ulinzi aliyekuwa anashikiliwa na kundi hilo.
Mgogoro wa kisiasa na kiusalama nchini Côte d’Ivoire uliibuka kufuatia malalamiko ya askari waasi kuanza kufyatua ovyo risasi katika miji muhimu ya taifa hilo. Baadhi ya askari hao waliokuwa wanalalamikia nyongeza ya mishahara yao, walikuwa wanaratibu pia mgomo wa nchi nzima wa wafanyakazi wa serikali sambamba na kufyatua risasi angani na kufunga barabara za kuingilia miji kadhaa.
Awali malalamiko ya waasi hao yalianzia katika mji wa Bouaké na kuenea miji mingine mikubwa ukiwemo Abidjan, ambao ni mji mkuu wa kiuchumi na kibiashara wa nchi hiyo. Baada ya askari hao kukataa pendekezo la Rais Alassane Ouattara, juzi usiku walizingira makazi ya Alain Richard Donwahi, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo mjini Bouaké alikokuwa ameenda kwa ajili ya kuzungumza nao sambamba na kumzuia kutoka eneo hilo. Hata hivyo saa chache baadaye askari hao waasi walimuachilia huru waziri huyo. Hata kama ni miaka kadhaa sasa tokea Ivory Coast ipige hatua katika kuboresha demokrasia na uchumi, lakini bado nchi hiyo inakabiliwa na matatizo ya uthabiti na kiusalama. Hata kama askari wa nchi hiyo wanahesabika kuwa wafuasi wa Rais Alassane Ouattara, lakini bado kuna mambo ambayo wamekuwa wakitaka yatekelezwe na serikali yake.
Rais Ouattara ametangaza kuwa yuko tayari kuongeza mishahara ya askari hao, kudhamini makazi na kuboresha hali yao ya maisha. Hivi sasa mazingira ya uchumi ya Ivory Coast yameboreka, lakini pamoja na hayo miundomsingi ya uchumi bado sio ya kuridhisha. Licha ya kwamba nchi za Magharibi hususan Ufaransa zimekuwa na uingiliaji nchini humo, lakini hazitekelezi majukumu yao katika kutatua matatizo ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Miongoni mwa nara alizozitoa rais wa nchi hiyo katika kipindi cha uchaguzi wa rais uliopita, ni kufuatilia hali ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa fursa za ajira kwa lengo la kupunguza ukosefu wa kazi, mfumuko wa bei na umasikini nchini humo.
Ni kwa ajili hiyo ndio maana utendaji kazi wake ukatiliwa shaka hususan katika sekta ya uchumi. Kando na mahitaji ya kiuchumi, baadhi ya jumuiya na vyama vya siasa, vinalalamikia mwenendo wa kisiasa wa serikali ya Yamoussoukro. Kufanyika uchaguzi wa rais na bunge miezi kadhaa iliyopita, ni nukta muhimu inayotajwa kuwa imetekelezwa kwa ajili ya kurejesha usalama na uthabiti wa kisiasa nchini Ivory Coast. Hata hivyo wapinzani wameendelea kukosoa baadhi ya siasa za rais huyo. Akthari ya wapinzani wanatilia shaka msimamo huru wa Rais Alassane Ouattara. Wanasema kuwa rais huyo ameikabidhi Côte d’Ivoire kwa Wafaransa. Hali ikiwa ni hiyo, pande zingine zinataka kuimarishwa usalama na uthabiti wa kisiasa wa taifa hilo hususan katika mipaka yake na nchi nyingine. Wengi wa wapinzani wa rais huyo ni wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Laurent Gbagbo, ambao wanataka kurejea kwake madarakani. Hata kama mgogoro wa hivi karibuni unaonekana kumalizika, lakini endapo Rais Ouattara hatoweza kutekeleza ahadi zake sanjari na kutotekeleza matakwa ya askari na raia wa nchi hiyo, kuna uwezekano wa kuibuka upya machafuko dhidi ya serikali yake.