ANC: Wanaokutana na Waziri Mkuu wa Israel ni wahaini
Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC kimepinga vikali hatua ya kiongozi wa chama cha upinzani ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kusema kuwa huo ni uhaini.
Taarifa iliyotolewa na chama cha ANC kuhusu tukio hilo imesema kuwa: Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Democratic Alliance, Mmusi Maimane amesaliti tangazo la Mzee Nelson Mandela la udharura wa kushikamana na watu wanaokandamizwa wa Palestina kwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Chama tawala nchini Afrika Kusini kimesema, hatua hiyo ya wapinzani ni sawa na kupasisha ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Israel na kuuunga mkono utawala huo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hatua hiyo ni kinyume na juhudi za kimataifa za kuonesha mshikamano na watu wa Palestina.
Afrika Kusini inatambua sera na siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina kuwa ni sawa na sera za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zikitekelezwa na utawala wa makuburu nchini humo kati ya mwaka ya 1948 na 1994.