Wahanga wa shambulizi la ash-Shabab Somalia waongezeka na kufikia 83
(last modified Thu, 26 Jan 2017 07:33:49 GMT )
Jan 26, 2017 07:33 UTC
  • Wahanga wa shambulizi la ash-Shabab Somalia waongezeka na kufikia 83

Watu 83 wameripotiwa kuuawa katika shambulizi la kigaidi lililotekelezwa jana na wanachama wa genge la ash-Shabab lenye mafungamano na kundi la al-Qaidah huko Somalia.

Shambulizi hilo lililotokea katika lango la kuingilia katika hoteli ya Dayah, karibu na bunge na ikulu ya rais wa Somalia limetajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2017. Abdul-Qadir, mkuu wa idara ya masuala ya dharura nchini Somalia amesema kuwa awali mtu aliyekuwa akiendesha gari lililokuwa limetegwa ndani yake mabomu aliligongesha kwenye lango la hoteli hiyo na kusababisha watu 13 kuuawa na kwamba baada ya hujuma hiyo wanachama wanne wa genge hilo waliokuwa wamejizatiti kwa silaha waliingia hotelini na kuanza kuwamiminia risasi watu waliokuwa eneo hilo.

Hoteli ya Dayah baada ya kushambuliwa

Umoja wa Waandishi wa habari nchini Somalia umesema kuwa, katika hujuma ya pili, waandishi wa habari kutoka mashirika ya habari ya Ufaransa, Associated Press na televisheni ya Al-Jazira, wamejeruhiwa. Muda punde baadaye kundi hilo lilitangaza kuhusika na hujuma hiyo. Kundi la kigaidi la al-Shabab limekuwa likiendesha harakati zake za kigaidi nchini Somalia tangu mwaka 2007 kwa lengo la kuing'oa madarakani serikali ya nchi hiyo.

Majeruhi wa hujuma hiyo

Mwaka 2011 kundi hilo lilifanikiwa kudhibiti mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na Afgooye. Hata hivyo operesheni za jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa AMISOM zilifanikiwa kuwatimua wanachama wa kundi hilo kutoka maeneo hayo.

Tags