Al-Shabaab yadai kuua askari 66 wa KDF Somalia, Kenya yakanusha
(last modified Fri, 27 Jan 2017 13:46:19 GMT )
Jan 27, 2017 13:46 UTC
  • Al-Shabaab yadai kuua askari 66 wa KDF Somalia, Kenya yakanusha

Jeshi la Kenya limekadhibisha madai yaliyotolewa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kwamba limeua makumi ya wanajeshi wa KDF katika kambi ya jeshi iliyoko katika mji wa Kulbiyow, kusini mwa Somalia.

Msemaji wa al-Shabaab amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akidai kuwa, wanachama wa magaidi hao wameshambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya walioko Somalia chini ya mwavuli wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM, katika mji wa Kulbiyow, na kufanikiwa kuua askari 66 wa Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF.

Hata hivyo, msemaji wa KDF, Luteni Kanali Paul Njuguna amekanusha madai hayo aliyoyataja kuwa ya kipropaganda na kufafanua kuwa, wanajeshi wa Kenya katika kambi hiyo wamefanikiwa kuzima hujuma hiyo ya al-Shabaab leo Ijumaa na kwamba idadi kubwa ya wafuasi wa kundi hilo la kigaidi wameuawa.

Askari wa Amisom wakishika doria nchini Somalia

Hii ni katika hali ambayo, milipuko miwili ya juzi iliyotokeka baada ya malori mawili yaliyotegwa mabomu kulipuka katika hoteli ya Dayah karibu na Bunge na Ikulu ya Rais mjini Mogadishu, iliua watu 32 na kujeruhi wengine 51.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo tangu mwaka 2007 linapigana na kufanya hujuma mbalimbali ili kuing'oa madarakani serikali ya Somalia mwaka 2011 lilipoteza udhibiti wa mji mkuu na wa baadhi ya ngome zake zingine kama vile mji wa Afgoye.

Ikumbukwe kuwa, wanajeshi zaidi ya 100 wa KDF waliripotiwa kuuawa katika shambulizi jingine la al-Shabaab katika kambi ya jeshi la Kenya nchini Somalia mjini El-Adde, Januari mwaka jana, karibu na mpaka wa nchi mbili hizo. 

Tags