Al-Shabaab yawachinja 'majasusi' wa Kenya na US hadharani
(last modified Mon, 06 Feb 2017 07:47:46 GMT )
Feb 06, 2017 07:47 UTC
  • Al-Shabaab yawachinja 'majasusi' wa Kenya na US hadharani

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limewaua kwa kuwakata vichwa watu wanne wanaoshukiwa kuwa majasusi, kusini mwa Somalia.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu Mohamed Abu Abdalla, Gavana wa eneo la Jubba lililoko chini ya udhibiti wa al-Shabaab akisema kuwa, watuhumiwa hao wa ujasusi waliuawa jana Jumapili katika wilaya ya Jamame, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya serikali kuu ya Mogadishu, Kenya na Marekani.

Mahakama ya kundi hilo la kigaidi katika wilaya ya Jamane, kusini mwa eneo la Jubba inadaiwa kutoa hukumu hiyo ya kunyongwa watuhumiwa hao baada ya wenyewe kukiri kuwa walikuwa majasusi.

Magaidi wa al-Shababaab wakisoma taarifa kabla ya kutekeleza hukumu ya kifo

Hukumu hiyo ilitekelezwa adhuhuri ya jana Jumapili, katika eneo la Jubba linalodhibitiwa na kundi hilo la kigaidi na kitakfiri, yapata kilomita 70 kaskazini mwa Kismayu, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Hii sio mara ya kwanza kwa al-Shabaab kutekeleza unyama huo mbele ya familia na watu wa karibu na wahanga wa jinai zao hizo za kutisha.

Mwezi Novemba mwaka jana, wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi hilo la kigaidi, eti kwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutolipa kodi na zaka wanazotozwa kwa nguvu na al-Shabaab.

Tags