UN Yaikosoa Burundi kwa kupiga marufuku asasi za kiraia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24797-un_yaikosoa_burundi_kwa_kupiga_marufuku_asasi_za_kiraia
Jopo la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa limelaani marufuku na kusimamishwa kwa muda kwa asasi za kiraia, iliyotolewa hivi karibuni na serikali ya Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2017 00:51 UTC
  • UN Yaikosoa Burundi kwa kupiga marufuku asasi za kiraia

Jopo la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa limelaani marufuku na kusimamishwa kwa muda kwa asasi za kiraia, iliyotolewa hivi karibuni na serikali ya Burundi.

Katika taarifa ya Jumatatu, jopo hilo limeonya kuhusu kile lilichokitaja kuwa madhara ya vizuizi na unyanyapaa unaotokana na sheria dhidi ya asasi za kiraia na kusema sera hizo zinalenga kukandamiza watetezi wa haki za binadamu.

Taarifa ya wataalmu hao inafuatia marufuku dhidi ya asasi tano za kiraia iliyotolewa Oktoba 19 mwaka jana, na kufuatiwa na marufuku dhidi ya ITEKA ambayo ni miongoni mwa asasi za kiraia za haki za binadamu inayoongoza Burundi, huku pia asasi nyingine inayoitwa OLUFAD inayotetea utawala bora na kupinga rushwa ikipigwa marufuku.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Kwa mujibu wa watalaamu hao wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, bunge la nchi hiyo lilipitisha sheria baada ya marufuku hizo, sheria zilizolenga kuzidhibiti asasi za kiraia za kitaifa na kimataifa ikizitaka kupata idhini ya kazi zao kwa waziri wa mambo ya ndani pamoja na kuhamisha fedha kutoka nje kupitia benki kuu. Wamesema kuwa hatua hizo ambazo ni mfululuzo wa kuzorota kwa haki za binadamu nchini Burundi, zinaendeleza madhila kwa watetezi wa haki hizo na kuongeza kuwa wale ambao hawajaondoka nchini humo wanahofia maisha yao huku wakitishiwa kuwekwa kizuizini, kuteswa na kutoweka.