EU: Tutaipatia Gambia msaada wa Euro milioni 75 ili kujidhaminia chakula
Neven Mimica, Kamishna wa Ushirikiano na Ustawi wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, umoja huo utaisaidia serikali ya Gambia msaada wa kiasi cha Euro milioni 75.
Mimica ameyasema hayo mjini Banjul, mji mkuu wa Gambia wakati alipokutana na Rais Adama Barrow wa nchi hiyo na kwamba msaada huo utasaidia kutatua matatizo ya chakula, ukarabati wa barabara na kuanzisha fursa za ajira nchini humo.

Matamshi hayo ya Kamishna wa Ushirikiano na Ustawi wa Umoja wa Ulaya yanakuja ikiwa ni wiki chache zimepita tangu kuondoka madarakani rais wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh. Itakumbukwa kuwa misaada ya EU kwa nchi hiyo ilisimamishwa mwishoni mwa mwaka 2014, kutokana na baadhi ya misimamo ya rais huyo wa zamani ambaye kwa sasa yuko uhamishoni. Kabla ya hapo pia Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, itaanza kuchunguza jinsi ya kuisaidia Gambia, kwa ajili ya kuboresha hali yake ya kifedha, uchumi na hali ya mabenki ya nchi hiyo masikini ya magharibi mwa Afrika.

Yahya Jammeh aliyeitawala Gambia kwa kipiundi cha miaka 22 aliondoka madarakani wiki chache zilizopita kutokana na mashinikizo ya walimwengu, baada ya hatua yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe Mosi Disemba, ambayo awali aliyakubali.