Feb 10, 2017 08:07 UTC
  • Viongozi wa Kiislamu Tanzania waunga mkono vita dhidi ya mihadarati

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania Alhad Mussa Salum amesema dawa za kulevya zinateketeza nguvukazi ya taifa, jambo ambalo halipaswi kuachwa liendelee kumea.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Sheikh Alhad amesema Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya nchini linaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kwa ajili ya kupambana na jambo hilo.

Gazeti la Mwananchi la Tanzania limemnukuu kiongozi huyo wa kidini akisema kuwa: “Suala la matumizi ya dawa za kulevya limekuwa kikwazo cha maendeleo nchini kutokana na nguvu kubwa ya taifa ambayo ni vijana kujihusisha na utumiaji wa dawa hizo.” 

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum 

Amesema kuwa wanawataka viongozi wengine wa umma kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wa kupambana na uovu wa uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambao ni janga kwa taifa.

Katibu wa Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Mihadarati nchini Tanzania, Padri John Solomoni ameitaka serikali kushughulikia suala hilo kwa umakini ili lisiibue manung’uniko miongoni mwa wananchi ambao hawana hatia.

Kwa takriban wiki moja sasa, watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, wasanii wafanyabiashara wamehojiwa na polisi ya Tanzania kuhusiana na ama utumiaji wa dawa hizo au uuzaji katika vita vinavyoendeshwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

 

Tags