Waafrika Kusini watakiwa kukomesha mashambulizi dhidi ya wageni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25552-waafrika_kusini_watakiwa_kukomesha_mashambulizi_dhidi_ya_wageni
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini amewataka wananchi wa nchi hiyo kuwa watulivu kufuatia ghasia na machafuko yanayowalenga wahajiri na raia wa nchi za kigeni nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 23, 2017 23:37 UTC
  • Waafrika Kusini watakiwa kukomesha mashambulizi dhidi ya wageni

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini amewataka wananchi wa nchi hiyo kuwa watulivu kufuatia ghasia na machafuko yanayowalenga wahajiri na raia wa nchi za kigeni nchini humo.

Malusi Gigaba amesema serikali ya Pretoria inafanya jitihada za kukomesha machafuko na vitisho na amewataka raia wote wa nchi hiyo kusitisha mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini pia ameahidi kwamba serikali ya nchi hiyo itashughulikia tatizo hilo na kuheshimu sheria zunazohusiana na haki za wahajiri na raia wa kigeni. 

Matamshi hayo yametolewa baada ya wimbi jipya la hujuma na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya wahajiri na raia wa kigeni katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Majumba kadhaa ya raia wa kigeni katika miji ya Afrika Kusini hususan Pretoria na Johannesburg yamechomwa moto na kushambuliwa katika siku kadhaa za hivi karibuni.

Rais wa kigeni wanashambuliwa na kupigwa Afrika Kusini

Jumuiya ya Kimataifa ya Wahajiri imelaani mashambulizi hayo yanayochochewa na chuki dhidi ya wageni na kusisitiza kuwa hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa raia wa kigeni ndiyo sababu ya kuongezeka uhalifu nchini Afrika Kusini.