Asasi ya kiraia Burundi: Tuna wasi wasi wa hatma ya watu waliotoweka
Asasi za kiraia nchini Burundi zimeonyesha wasi wasi wao juu ya hatma ya watu waliotoweka katika kipindi cha mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Pacifique Nininahazwe, mmoja wa wanaharakati wa kiraia nchini Burundi sambamba na kuonyesha wasi wasi wake juu ya hali isiyojulikana na watu waliotoweka katika kipindi cha mgogoro nchini humo amesema kuwa hadi sasa hakuna habari zozote za kutia moyo katika uwanja huo. Kutokana na hali hiyo taasisi ya masuala ya kibinaadamu maarufu kwa jina la FOCODE, imeanzisha mpango uliopewa jina la NDONDEZA kwa ajili ya kuwatafuta watu waliotoweka nchini Burundi.
Nininahazwe ameikosoa serikali ya Bujumbura hususan Wizara ya Sheria na idara ya usalama wa taifa ya nchi hiyo kwa kutotoa radiamali ya maana katika uwanja huo. Mgogoro wa Burundi ambao sasa unakaribia miaka miwili, umekumbwa na vitendo vya uvunjaji wa haki za binaadamu ambapo hadi sasa karibu watu 1000 wameuawa, maelfu ya wengine kuwa wakimbizi, mamia kutiwa nguvuni huku wengine wakitoweka katika mazingira ya kutatanisha. Hii ni katika hali ambayo Mahakama ya kimataifa ya jinai imeanzisha uchunguzi wa ukiukaji wa haki za binaadamu nchini Burundi.