Bunge la Somalia lamuidhinisha Waziri Mkuu mpya, aahidi kutokomeza ufisadi
Bunge la Somalia limemuidhinisha Hassan Ali Khaire kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo katika kikao cha ufunguzi wa Bunge la 10 leo Jumatano, kilichofunguliwa na Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo.
Kati ya wabunge 299 walioshiriki kikao cha leo chini ya uenyekiti wa Spika Mohamed Osman Jawari, 231 wamepiga kura ya kuunga mkono uteuzi wa Khaire huku wawili wakijizuia. Baada ya kuidhinishwa, aliapishwa katika majengo ya Bunge na Rais wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo.
Khaire, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Mafuta na Gesi la Soma la Uingereza na ambaye pia ana uraia wa Norway, aliteulwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na Rais Farmaajo wiki iliyopita.
Waziri Mkuu mpya wa Somalia ameahidi kushirikiana na Rais Farmaajo katika vita dhidi ya ufisadi na jinamizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.
Amekiambia kikao hicho cha Bunge kuwa: "Naahidi kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote aliyejihusisha au atakayepatikana anajihusisha na ufisadi."
Waziri Mkuu mpya wa Somalia kwa mashauriano na rais anatazamiwa kulitangaza baraza la mawaziri katika kipindi cha siku chache zijazo.