ANC yaahidi kutokomeza ufisadi Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26280-anc_yaahidi_kutokomeza_ufisadi_afrika_kusini
Chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, kimesema, kinapaswa kumaliza ufisadi na kukomesha mifarakano baina ya wanachama sambamba na kutekeleza ahadi za kuangamiza umaskini iwapo kinataka kusitisha mkondo wa sasa wa kupoteza umashuhuri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2017 10:13 UTC
  • Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini
    Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

Chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, kimesema, kinapaswa kumaliza ufisadi na kukomesha mifarakano baina ya wanachama sambamba na kutekeleza ahadi za kuangamiza umaskini iwapo kinataka kusitisha mkondo wa sasa wa kupoteza umashuhuri.

Kwa mujibu wa sera mpya za chama zilizotangazwa leo Jumapili, ANC imekiri inapoteza umashuhuri huku baadhi ya wanachama wake wakihamia chama kipya cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF). Chama hicho kinapendekeza kuwa ardhi zinazomilikiwa na makaburu, walowezi Wazungu, zichukuliwe kwa nguvu na kukabidhiwa wazalendo Waafrika.

Msemaji wa ANC, Zizi Kodwa amesema, sera mpya za chama zitatangazwa katika kongamano la kitaifa litakalofanyika mwezi Juni.

Mapema mwezi huu Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alipendekeza kuwa katiba ibadilishwe ili ardhi zinazomilikiwa na makabaru wapewe Waafrika pasina makaburu hao kupewa fidia.

Pendekezo hilo limepelekea chama cha EFF kupata uungaji mkono miongoni mwa wapiga kura masikini. Hata hivyo ANC imepinga pendekezo la EFF la kutaifishwa migodi na kuonya kuwa, hatua kama hiyo itapelekea idadi kubwa ya watu kupoteza kazi.