Mar 15, 2017 07:14 UTC
  • UN: S/Kusini, AU zakwamisha kubuniwa mahakama ya haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeilaumu serikali ya Juba na Umoja wa Afrika (AU) kuwa zinakwamisha juhudi za kubuniwa mahakama ya kuwapandisha kizimbani wavunjaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini.

Kenneth Scott, Afisa wa Uchunguzi katika Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema kuwa, serikali ya Rais Salva Kiir na Umoja wa Afrika zimekataa kata kata kushirikiana na UN kufanikisha mpango wa kubuniwa koti hiyo.

Amefafanua kuwa: "Tumeomba mafaili ya kesi ambayo tunajua wanayo, rasimu ya sheria na rasimu ya Mkataba wa Maelewano ili kwa pamoja tuandae ramani ya njia ya kubuniwa chombo hicho cha kisheria lakini wamekataa kutupa. La kusikitisha zaidi, baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wametuambia kuwa katu hilo haliwezekani kabisa. " 

Wananchi wa Sudan Kusini wakitoroka jinai za jeshi na waasi

Hivi karibuni, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ililaani vikali uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini na kusema kuwa, askari wa serikali wamefanya jinai za kibinadamu nchini humo.

Zeid Raad al-Hussein, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, uvunjaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini ni mbaya na mkubwa mno kuliko sehemu yoyote ile duniani na kwamba, uvunjaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini ni sawa na jinai za kivita.

Tags