UN yalalamikia utendaji wa serikali ya Burundi kuhusu haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26426-un_yalalamikia_utendaji_wa_serikali_ya_burundi_kuhusu_haki_za_binadamu
Umoja wa Mataifa umeilalamikia serikali ya Burundi kwa kutoshirikiana na umoja huo katika kuchunguza suala la haki za binadamu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 15, 2017 13:03 UTC
  • UN yalalamikia utendaji wa serikali ya Burundi kuhusu haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umeilalamikia serikali ya Burundi kwa kutoshirikiana na umoja huo katika kuchunguza suala la haki za binadamu nchini humo.

Fatsah Ouguergouz, Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu huko Burundi ameeleza kuwa kwa bahati mbaya viongozi wa serikali ya Bujumbura hawakutoa ushirikiano uliohitajika kwa kamati hiyo kwa ajili ya kutambua hali waliyo nayo wahanga wa ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo. 

Fatsah Ouguergouz ameongeza kuwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vingali vinatia wasiwasai huku Burundi licha ya kuachiwa huru baadhi ya wafungwa wa kisiasa. Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu nchini Burundi amebainisha kuwa serikali ya Bujumbura imewasilisha taarifa kuhusu uamuzi wake wa kujiondoa katika mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), hata hivyo kamati hiyo inaendelea na shughuli zake na itafuatilia pia masuala ya kisheria yanayohitajika.

Fatsah Ouguergouz, Mkuu wa Kamati ya Uchunguzi ya UN kuhusu Haki za Binadamu huko Burundi  

Kwa mujibu wa matamshi ya mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Burundi tarehe Tatu Januari mwaka huu iliwaachia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa, hata hivyo wawakilishi wa taasisi za kijamii, waandishi habari na wanasiasa wa upinzani wa nchi hiyo wanaikimbia nchi kwa kuhofia kutiwa nguvuni. Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa tangu mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya Rais Piere Nkurunziza wa nchi hiyo kutangaza azma yake ya kuendelea kusalia madarakani kinyume na katiba.