UN: Sudan Kusini inawahamisha watu kwa msingi wa kikabila
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26450-un_sudan_kusini_inawahamisha_watu_kwa_msingi_wa_kikabila
Serikali ya Sudan Kusini imeanza kampeni ya kuorodhesha na kuhamisha watu kwa mujibu wa makabila yao.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 16, 2017 03:44 UTC
  • UN: Sudan Kusini inawahamisha watu kwa msingi wa kikabila

Serikali ya Sudan Kusini imeanza kampeni ya kuorodhesha na kuhamisha watu kwa mujibu wa makabila yao.

Hayo yamedokezwa na mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Yasmin Sooka ambaye pia ni mwenyekiti wa tume Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa haki za binadamu Sudan Kusini.

Akizungumza kwenye Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva Yasmin Sooka amesema wakati vita vya wenyewe kwa wenye vikiendelea nchini humo, kitendo cha serikali kuchora upya mipaka kimepunguza idadi ya watu wa kabila la Shilluk na Nuer kwenye jimbo la Upper Nile.

Ameongeza kuwa, ripoti zinaonyesha kwamba raia wa Sudan Kusini wanalengwa kwa makusudi kwa misingi ya kabila na wanajeshi wa serkali ambao wanawaua, kuwatekwa nyara, kuwashikilia kiholela na kuwanyima uhuru wao. Aidha amesema vikosi vya jeshi la serikali  vinawabaka raia sambamba na kuteketeza vijiji na kupora mali za raia.

Askari watiifu kwa serikali ya Sudan Kusini

Mwezi Novemba mwaka jana mtaalamu wa Umoja wa Mataifa alionya kuwa, yumkini Sudan Kusini ikatumbukia katika mauaji ya kimbari kutokana na kushadidi mapigano ya kikabila nchini humo.

Adama Dieng, mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kuzuia mauaji ya kimbari amesema kuwa, wimbi la mauaji ya kikabila linaloshuhudiwa nchini Sudan Kusini kwa sasa linatia wasiwasi.