UNHCR yatahadharisha kuhusu janga la wakimbizi wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26564-unhcr_yatahadharisha_kuhusu_janga_la_wakimbizi_wa_sudan_kusini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limeshtushwa na idadi kubwa ya raia wa Sudan Kusini wanaokimbia makaazi yao na kuelekea nchi jirani au kuwa wakimbizi ndani ya nchi.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 19, 2017 00:37 UTC
  • UNHCR yatahadharisha kuhusu janga la wakimbizi wa Sudan Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema limeshtushwa na idadi kubwa ya raia wa Sudan Kusini wanaokimbia makaazi yao na kuelekea nchi jirani au kuwa wakimbizi ndani ya nchi.

Katika taarifa  UNHCR imesema watu waliotawanywa Sudan Kusini na kuingia katika nchi jirani ni milioni 1.6 huku kiwango kipya cha wakimbizi kikitia hofu. Shirika hilo linasema hakuna nchi ya jirani iliyo na kinga kwani wakimbizi wanaingia, Uganda, Sudan, Ethiopia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), sasa mataifa hayo ambayo pia yana matatizo yake yanasema yamezidiwa na yanahitaji msaada ili kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao.

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch  anasema kufikia sasa ufadhili kwa ajili ya wakimbizi wa Sudan Kusini katika eneo zima ni asilimia 8 tu kutoka kiwango kinachohitajika cha dola milioni 781. Amesema  UNHCR inahitaji dola milioni 250 kukabiliana na hali ya njaa na ongezeko la wakimbizi Sudan Kusini.

Haya yanakiri wakati ambao, ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema: Serikali ya Sudan Kusini ndiyo inayobeba lawama kubwa kwa baa la njaa linaloshuhudiwa katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo huku Rais wa nchi hiyo Salva Kiir akiendelea kutumia mamilioni ya dola zinazotokana na mauzo ya mafuta kuimarisha vikosi vyake vya ulinzi.

Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la mapinduzi. 

Takwimu zinaonesha kuwa, sasa asilimia 42 ya watu wote wa Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na matatizo hayo ya kiuchumi, vita vya ndani na kusambaratika kwa sekta ya kilimo.