Ndege ya abiria yaanguka ikiwa na watu 45 Sudan Kusini
Ripoti kutoka Sudan Kusini zinasema ndege moja ya abiria iliyokuwa na wasafiri 40 na wahudumu 5 imeanguka katika uwanja wa ndege wa Wau.
Ndege hiyo imeanguka wakati ilipokuwa ikitua katika uwanja wa mji wa Wau.
Ripoti za awali zilidai kuwa watu wote 45 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wamefariki dunia lakini meneja wa South Supreme Airlines ameviambia vyombo vya habari kwamba, hakuna mtu aliyefariki dunia katika ajali hiyo. Ameongeza kuwa watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo wameondolewa ndani yake kabla haijashika moto na kuanza kuungua.
Mwandishi habari James Dimo Deng aliyeshuhudia tukio hilo amesema abiria 18 wamejeruhiwa na kwamba wamehamishiwa hospitalini.
Picha kutoka Sudan Kusini zimeonesha ndege hiyo ya abiria ikiteketea kwa moto.
Maafisa wa serikali ya Sudan Kusini wanasema ndege hiyo aina ya Antonov AN-26 ilikuwa ikitokea katika mji wa nchi hiyo, Juba.