Mar 22, 2017 16:06 UTC
  • Wimbi la mashambulizi ya kigaidi laua na kujeruhi 28 Maiduguri, Nigeria

Kwa akali watu wanane wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika wimbi la hujuma za kigaidi lililoutikisa mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria mapema leo.

Shirika la Taifa la Kukabiliana na Dharura la Nigeria limethibitisha kutokea miripuko kadhaa katika mji huo, ambao ni moja ya ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi watano wa kujitolea muhanga wanaoaminika kuwa wanachama wa genge hilo la kigaidi ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi hayo.

Damian Chukwu, Kamishna wa Polisi katika Jimbo la Borno ameliambia shirika la habari Reuters kuwa, hujuma hizo zilitokea saa kumi na nusu alfajiri ya leo, na miripuko mitatu kati ya mitano iliyotokea imeripotiwa katika karakana ya magari mjini Maiduguri.

Moja ya miripuko iliyotokea mjini Maiduguri

Inaarifiwa kuwa, watu zaidi ya 20 wamejeruhiwa katika msururu wa mashambulizi hayo ya mabomu, katika barabara kuu ya Maiduguri-Gamboru leo asubuhi.

Jumapili iliyopita, miripuko mitatu ya kigaidi iliyotokea katika kijiji kimoja kilichoko karibu na mji wa Maiduguri iliua watu wasiopungua wanne na kujeruhi wengine wanane.

Mwezi uliopita, watu 11 waliuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags