UN yataka kuongezwa juhudi za kutatua mgogoro wa Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26742-un_yataka_kuongezwa_juhudi_za_kutatua_mgogoro_wa_sudan_kusini
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuongezwa juhudi za kuutatua mgogoro wa Sudan Kusini na kusisitiza kuwa mazungumzo ya kisiasa ndiyo njia pekee ya kumaliza machafuko nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2017 03:11 UTC
  • UN yataka kuongezwa juhudi za kutatua mgogoro wa Sudan Kusini

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuongezwa juhudi za kuutatua mgogoro wa Sudan Kusini na kusisitiza kuwa mazungumzo ya kisiasa ndiyo njia pekee ya kumaliza machafuko nchini humo.

Hervé Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Usimamiaji Amani wa umoja huo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hayo huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini na kuongeza kuwa, matumizi ya silaha hayawezi kumaliza mgogoro huo.

Aidha ameashiria mazungumzo yake na Rais Salva Kiir wa Sudani Kusini na kusema kuwa hali ya kiusalama nchini humo inatia wasiwasi mkubwa. Amesema, idadi kubwa ya watu wanaolazimika kukimbia makazi yao kutokana na usalama mdogo, ni onyo kubwa kwa serikali ya Sudan Kusini.

Hervé Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Usimamiaji Amani

 

Wakati huo huo Rwanda imesema kuwa, iko tayari kutuma askari zaidi Sudan Kusini. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi na masuala ya kijeshi wa nchi hiyo, Luteni Kanali René Ngendahimana amesema kuwa, Kigali inajiandaa kutuma askari zaidi wa kulinda amani nchini Sudan Kusini chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha UNMISS.

Alisema hayo jana baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kusimamia amani Hervé Ladsous kusema kwamba, kundi la kwanza la askari wa kulinda amani kutoka Rwanda, Nepal na Bangladesh litaanza kuwasili Sudan Kusini wiki chache zijazo.