Apr 05, 2017 04:10 UTC
  • Muungano wa vyama vya wafanyakazi Afrika Kusini wamtaka Zuma ajiuzulu

Shirikisho Kuu la Vyama vya Wafanyakazi Afrika Kusini (Cosatu) limemtaka Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo aachie ngazi likisisitiza kuwa mwanasiasa huyo amepoteza itibari na uwezo wa kuliongoza taifa.

Bheki Ntshalintshali, Katibu Mkuu wa shirikisho hilo amesema Zuma anafaa kujiuzulu mara moja kutokana na hatua yake ya kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri, kitendo ambacho kilipelekea kupigwa kalamu nyekundu Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Pravin Jamnadas Gordhan.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho Kuu la Vyama vya Wafanyakazi Afrika Kusini, Sidumo Dlamini ametishia kuwa, muungano huo wenye ushawishi mkubwa wa wafanyakazi utaitisha maandamano ya nchi nzima kumshinikiza Zuma ajiuzulu iwapo atakataa kuondoka madarakani kwa khiari.

Gordhan alifutwa kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Malusi Nkanyezi Gigaba. Kadhalika Rais Jacob Zuma alimfuta kazi Naibu Waziri wa Fedha, Mcebisi Jonas na nafasi yake kuchukuliwa na Sifiso Buthelezi.

Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini aliyefutwa kazi, Pravin Gordhan

Vyama vingi vya siasa kikiwemo chama cha kikomonisti chenye ushirika na chama tawala nchini Afrika Kusini, vimekosoa uamuzi wa Rais Zuma wa kumfuta kazi Pravin Jamnadas Gordhan na kuitaja hatua hiyo kuwa ni ya kidikteta.

Kadhalika mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri yamefichua mpasuko na msuguano mkubwa ndani ya chama tawala (ANC), baadhi ya wanachama wakiunga mkono hatua hiyo ya Zuma na wengine wakiikosoa vikali. 

Cyril Ramaphosa, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini ambaye pia ni naibu kinara wa ANC amenukuliwa na vyombo vya habari akisema: "Kuna baadhi ya wanachama wetu hawajafurahia mabadiliko hayo, hususan hatua ya kufutwa kazi Gordhan, ambaye amelitumikia taifa hili kwa moyo wa kujituma na kujitolea."

Tags