Apr 05, 2017 16:10 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika mripuko wa kigaidi Somalia

Mripuko wa kigaidi ulioukumba mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, umeua watu kadhaa.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Nur Aden, mmoja wa maafisa wa polisi wa Somalia akisema kuwa mripuko huo umetokea leo (Jumatano) katika mkahawa mmoja karibu na Wizara za Usalama na Michezo katikati ya Mogadishu na kupelekea raia wasiopungua saba kuuawa.

Amesema, mripuko huo umefanya uharibifu kwenye mkahawa huo pamoja na mkahawa wa jirani na magari matatu yameharibiwa na mripuko huo mkubwa.

Miripuko ya mabomu mgogoro mkubwa nchini Somalia

 

Mripuko huo umetokea katika hali ambayo Mohamed Abukar Islow, waziri mpya wa masuala ya usalama wa Somalia ameahidi kuchukua hatua kali za kuimarisha usalama nchini humo.

Hadi hivi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la leo. Hata hivyo katika miaka ya huko nyuma, kundi la kigaidi la al Shabab ambalo ni tawi la mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ya aina hiyo katika maeneo mbalimbali ya Somalia na nje ya Somalia kiasi kwamba miripuko mingi inayotokea nchini Somalia na katika nchi jirani huwa inahusishwa moja kwa moja na kundi hilo la kigaidi.

Nchi jirani ya Kenya ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi wa al Shabab. 

Tags