Maelfu ya Waafrika Kusini kuandamana leo kushinikiza Rais Zuma ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27396-maelfu_ya_waafrika_kusini_kuandamana_leo_kushinikiza_rais_zuma_ajiuzulu
Maelfu ya watu wanatazamiwa kuandamana leo katika miji mikubwa ya Afrika Kusini dhidi ya Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma wakimtaka ajiuzulu baada ya mabadiliko aliyolifanyia Baraza la Mawaziri ambayo yamezusha mgogoro mpya kwa uongozi wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2017 00:12 UTC
  • Maelfu ya Waafrika Kusini kuandamana leo kushinikiza Rais Zuma ajiuzulu

Maelfu ya watu wanatazamiwa kuandamana leo katika miji mikubwa ya Afrika Kusini dhidi ya Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma wakimtaka ajiuzulu baada ya mabadiliko aliyolifanyia Baraza la Mawaziri ambayo yamezusha mgogoro mpya kwa uongozi wake.

Uamuzi uliochukuliwa Alkhamisi ya wiki iliyopita na Zuma wa kumtimua waziri wa fedha mwenye kuheshimika Pravin Gordhan umewakasirisha wapinzani na waungaji mkono wake na kudhoofisha nafasi yake mbali na kusababisha mpasuko ndani ya chama chake tawala cha ANC ambacho kinaiongoza Afrika Kusini tangu mwaka 1994 baada ya kuhitimishwa enzi za utawala wa wazungu wachache.

Wakala wa Viwango Duniani umekutaja kufutwa kazi Gordhan kama moja ya sababu za kuporomoka itibari ya kiuchumi ya Afrika Kusini, ambapo tangu Machi 27 pale Rais Zuma alipomwamuru Pravin Gordhan arudi nchini kutoka ughaibuni alikokuwa, sarafu ya nchi hiyo ya randi imeshuka kwa asilimia 11. Waziri huyo wa fedha wakati huo alikuwa amekwenda kufanya mazungumzo na wawekezaji.

Asasi ya kiraia iitwayo Okoa Afrika Kusini inatazamiwa kuongoza maandamano yatakayofanyika katika mji mkuu Pretoria. Asasi hiyo inajumuisha makundi ya kiraia, viongozi wa wafanyabiashara na shakhsia binafsi wanaoheshimika.

Kampeni za kumshinikiza Rais Jacob Zuma ajiuzulu

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Muungano wa Kidemokrasia (DA) Mmusi Maimane amesema chama hicho kitaongoza maandamano yatakayofanyika kwenye mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo Johannesburg huku maandamano mengine yakitazamiwa kufanyika katika miji ya Cape Town na Durban.

"Tunatoa wito kwa Waafrika Kusini wote bila kujali mafungamano au mielekeo yao ya kisiasa kujiunga na hatua hii ya umma kwa ajili ya mabadiliko ambapo tutasimama pamoja na kutamka kwa sauti moja kwamba 'Zuma lazima aondoke na Afrika Kusini lazima ndio iwe kwanza'", amesisitiza kiongozi huyo wa upinzani…/