Wasi wasi wa Sudan kuhusu kuongezeka wimbi la wakimbizi wa Sudan Kusini
Serikali ya Sudan imeonyesha wasi wasi wake mkubwa juu ya mgogoro unaotokana na ongezeko la wakimbizi wa Sudan Kusini wanaoingia nchi hiyo.
Hamad Elgizouli, afisa wa masuala ya wakimbizi katika serikali ya Sudan amesema kuwa karibu kila siku wakimbizi 1500 raia wa Sudan Kusini wanaingia nchini Sudan kutokana na ukame, njaa kali na machafuko ya ndani ya nchi yao. Naye Noriko Yoshida, mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, zaidi ya wakimbizi elfu 60 kutoka Sudan Kusini hususan wanawake na watoto wameingia nchini Sudan ndani ya kipindi cha miezi mitatu pekee tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Hii ni katika hali ambayo Sudan yenye bado inakabiliwa na uhaba wa fedha na matatizo mbalimbali kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi hao. Noriko Yoshida amesema kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017, inakariwa jumla ya wakimbizi laki moja na elfu 80 raia wa Sudan Kusini wataingia nchini Sudan. Sudan Kusini ilitumbukia katika mgogo wa kisiasa mwaka 2013 baada ya Rais Salfa Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake wa rais kwamba alikula njama za kutaka kumpindua madarakani.