Kutangazwa Waziri Mkuu Mpya wa Kongo katika kutekeleza makubaliano ya kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27458-kutangazwa_waziri_mkuu_mpya_wa_kongo_katika_kutekeleza_makubaliano_ya_kisiasa
Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteua Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya kufanyika mashauriano ya kina na kuchelewa kuchukuliwa hatua hiyo.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Apr 08, 2017 11:13 UTC
  • Kutangazwa Waziri Mkuu Mpya wa Kongo katika kutekeleza makubaliano ya kisiasa

Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemteua Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo baada ya kufanyika mashauriano ya kina na kuchelewa kuchukuliwa hatua hiyo.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kumteua Bruno Tshibala mmoja wa viongozi wa upinzani kuwa Waziri Mkuu kupitia taarifa iliyorushwa na televisheni ya taifa ya nchi hiyo. Tshibala alikuwa msemaji wa chama kilichokuwa kikiongozwa na Etienne Tshisekedi kiongozi mashuhuri wa upinzani huko Kongo yaani chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), hata hivyo tarehe Mosi Februari alilalamikia ustahiki wa kupewa uongozi Felix Tshisekedi mwana wa kiume wa marehemu mzee Etienne Tshisekedi baada ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe; na ilipofika mwishoni mwa mwezi wa Februari, Bruno Tshibala alijiondoa kwenye chama hicho kilichoasisiwa na Tshisekedi.

Marehemu mzee Etienne Tshisekedi, aliyekuwa mwanasiasa mkongwe huko Kongo 

Tshibala alikuwa akitambulika kama mmoja wa viongozi wakuu wa chama hicho. Tshibala ameteuliwa ikiwa ni katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Disemba 31 mwaka jana kati ya wapinzani na serikali ya Kongo ili kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa unaoikabili. 

Mgogoro huo wa kisiasa umefika mbali sasa kufuatia kuakhirishwa uchaguzi wa Rais na vile vile kitendo cha Rais Joseph Kabila cha kung'ang'ania madaraka. Joseph Kabila ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuliwa baba yake Laurent Desire Kabila, alishinda katika chaguzi mbili za mwaka 2006 na 2011. Kwa vile duru ya uongozi wa Kabila ilipasa kumalizika mwezi Disemba mwaka jana, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, asingeweza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu. Hivyo Kabila alitangaza kuakhirisha uchaguzi wa rais na kusema kuwa atasalia madarakani hadi mazingira ya kufanyika uchaguzi mwingine yatakapoandaliwa. 

Hatua ya kuakhirisha uchaguzi wa Rais huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilizusha maandamano makubwa katika mji mkuu Kinshasa na kupelekea kuuawa makumi ya watu. Hatua hiyo pia iliwakasirisha wapinzani nchini humo. Wapinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanamtuhumu Rais Kabila kwamba anafanya sawa kabisa na baadh ya viongozi wengine wa nchi za Kiafrika walioamua kubaki madarakani milele. Wapinzani hao wanasema kuwa, kuakhirishwa uchaguzi wa rais kunampa fursa ya kutosha Joseph Kabila ya kuifanyia marekebisho katiba ili asiondoke uongozini.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokarsia ya Kongo 

Wakati huo huo baadhi ya makundi ya upinzani Kongo yanaamini kuwa uchaguzi wa rais umeakhirishwa nchini humo ili kumpa muda wa kutosha Rais Kabila wa kupanga mikakati ya kuiba kura. Jambo hilo limeshadidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo uliopelekea viongozi wa Kanisa Katoliki wa nchini humo waingilie kati na kusimamia mazungumzo mapana yaliyofanikisha kutiwa saini makubaliano kati ya serikali ya Kinshasa na wapinzani ili kuunda serikali ya mseto nchini humo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Kabila ataendelea kubakia katika hatamu za uongozi hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2017. Aidha imeamuliwa kuwa, baraza la mpito litakaloongozwa na kiongozi wa upinzani litaunda serikali na hata Waziri Mkuu alipaswa kuchaguliwa kutoka katika safu ya wapinzani.  Hata hivyo utekelezaji wa makubaliano hayo umechukua muda mrefu sana; jambo lililotarajiwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki huko Kongo. Kwa mujibu wa mpango wa utekelezaji wa makubaliano hayo, Waziri Mkuu alipaswa kuteuliwa mwezi Januari mwaka huu akitokea upande wa upinzani. Hata hivyo kuwepo mabishano kati ya serikali na wapinzani kuhusu namna ya kutekeleza makubaliano hayo na vile vile kuwepo hitilafu kubwa kati ya pande mbili hizo, yote hayo yamechelewesha utekelezaji wa vipengee vya makubaliano hayo. Kuteuliwa hivi sasa Waziri Mkuu Mpya huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka katika safu ya wapinzani tunaweza kuitaja kuwa ni hatua nyingine kuelekea utekelezaji kamili wa makubaliano ya Kongo yaliyofikiwa mwaka jana kati ya serikali na wapinzani na ni kuandaliwa uwanja maalumu wa kufanyika uchaguzi utakaohitimisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.