Apr 09, 2017 13:57 UTC
  • Wimbi la mlipuko wa mabomu dhidi ya makanisa laua makumi nchini Misri

Watu wasiopungua 140 wameuawa na kujeruhiwa katika wimbi la mashambulizi ya mabomu yaliyolenga makanisa nchini Misri hii leo.

Habari zinasema kuwa, kwa akali watu 26 wameuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa katika mlipuko wa kwanza wa bomu dhidi ya Kanisa la Kikhufti (Coptic) katika mji wa Tanta, eneo la Nile Delta.

Kanali ya televisheni ya serikali nchini Misri imeripoti kuwa, watu zaidi ya 45 wameuawa na kujeruhiwa katika mlipuko wa pili wa bomu uliolenga kanisa jingine katika mji wa Alexandria, kaskazini mwa nchi, masaa machache baada ya hujuma ya kwanza kuripotiwa mjini Tanta.

Timu za waokoaji zikinusuru manusura wa hujuma za kigaidi Misri

Maafisa wa serikali wamesema yumkini idadi ya waliouawa ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata wahanga wa hujuma hizo mbili zilizolenga waumini wa Kikiristo, ambao hii leo walikuwa wanaadhimisha Jumapili ya Matawi.

Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo. Magenge ya kigaidi yenye mafungamano na kundi hilo yamekuwa yakifanya hujuma za namna hii katika kona mbalimbali za nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Misri imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mabomu ya kundi la Ansar Baytul Muqaddas, tawi la genge la kigaidi la Daesh nchini humo, hujuma zilizoshadidi baada ya kundi hilo kutangaza utiifu wake kwa Daesh mwaka 2014.

Tags