Wapinzani Afrika Kusini waandamana; wamtaka Zuma aondoke madarakani
Maelfu ya watu leo Jumatano wameandamana huko Pretoria mji mkuu wa Afrika Kusini dhidi ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo kufuatia mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la mawaziri na kukabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani.
Maandamano ya leo huko Pretoria yamefanyika siku kadhaa baada ya mrengo wa upinzani kuitisha maandamano ya nchi nzima ya kumshinikiza Rais Zuma ajiuzulu. Wafanya maandamano wamezunguka mitaa yote ya mji mkuu Pretoria na kisha kufanya mkutano nje ya majengo ya Umoja; mahali ilipo ofisi ya Rais Jacob Zuma. Watu zaidi ya elfu sitini waliandamana pia Ijumaa iliyopita wakimtaka Rais Zuma aondoke madarakani, huku rais huyo akiwatuhumu baadhi ya waandamanaji kwa kudhihirisha vitendo vya kibaguzi.
Rais Zuma wa Afrika Kusini ambaye leo anatimiza umri wa miaka 75 huko nyuma alishawahi kukumbana na maandamano kama hayo. Hata hivyo chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) na vyama vingine vinavyoshiriki katika maandamano nchini vinaamini kuwa vina uwezo wa kuvutia uungaji mkono na hivyo kufanikisha kumuondoa uongozini Zuma baada ya kumfuta kazi Pravin Gordhan Waziri wa Fedha wa nchi hiyo aliyekuwa akiheshimiwa na matabaka mbalimbali nchini humo.