Wanafunzi karibu 20 wafariki dunia katika ajali ya barabarani Afrika Kusini
Dereva na watoto 19 wa shule wameaga dunia nchini Afrika Kusini wakati basi walilokuwa wakisafiria lilipogongana na lori na kulipuka kwa moto katika mkoa wa Mpumalanga.
Msemaji wa Idara ya Huduma za Dharura nchini Afika Kusini, Russel Meiring amesema kuwa gari hilo lilikuwa likisafirisha wanafunzi ilipogongana na lori kati ya miji ya Verena na Bronkhorstpruit, kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Pretoria.
Russel Meiring ameongeza kuwa, watoto kadhaa wa shule wamejeruhiwa katika ajali hiyo na kwamba baadhi yao wako katika hali mahututi.
Haikujulikana mara moja sababu ya ajali hiyo.
Japokuwa Afrika Kusini inatambuliwa kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na yenye mtandao wa barabara nyingi za kisasa, lakini pia imekuwa na rikodi mbaya sana ya usalama wa barabarani. Maafisa wa usafirishaji nchini humo wanasema kuwa, watu 235 walifariki dunia wakati wa Pasaka ya mwaka huu mwishoni mwa wiki ikilinganishwa na vifo 156 mwaka jana.