Sudan yamtuhumu Rais wa Sudan Kusini kwa kufanya mazungumzo na waasi
Sudan jana iliitaka nchi jirani ya Sudan Kusini isitishe uungaji mkono wake kwa makundi ya waasi wanaopigana vita na Khartoum na kumtuhumu Rais Kiir kuwa amekutana na kufanya mazungumzo na waasi wiki iliyopita.
Taarifa hiyo inatajwa kuwa ni nadra kutolewa na Idara ya Intelijinsia ya Khartoum.
Sudan mara kwa mara imekuwa ikiituhumu nchi jirani yake Sudan Kusini kuwa inawaunga mkono waasi katika majimbo ya Darfur, Blue Nile na Kordofan Kusini ambayo yanapakana na Sudan Kusini kwa upande wa Kusini.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenye vilivyochochea migawanyiko ya kikabila na mzozo wa kugombania maliasili tajiri ya mafuta.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Intelijinsia ya Sudan ni ya aina yake ambayo inamnyosheria kidole cha tuhuma moja kwa moja Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na hivyo kuibua uwezekano wa kushtadi hali ya mvutano kati ya nchi mbili hizo jirani.