Watu 20 wauawa katika mapigano ya kikabila Kasai, DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28310-watu_20_wauawa_katika_mapigano_ya_kikabila_kasai_drc
Watu wasiopungua 20 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea katika eneo la Kasai ya Kati huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2017 03:21 UTC
  • Watu 20 wauawa katika mapigano ya kikabila Kasai, DRC

Watu wasiopungua 20 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea katika eneo la Kasai ya Kati huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa Kongo DR MONUSCO imesema mapigano hayo yalitokea Aprili 19 mashariki mwa mji wa Tshikapa, makao makuu ya mkoa wa Kasai, kati ya watu wa makabila ya Lulua-Luba na Chowe-Pende.

Jamii ya Chowe-Pende ambayo aghalabu ya watu waliouawa wanatoka katika kabila hilo, inadai kuwa ndio mwenyeji asili wa eneo la Kasai, huku wakiwatuhumu watu wa kabila la Lulua-Luba kuwa wanaunga mkono waasi wa kundi la Kamuina Nsapu. 

Mauaji yanashuhudiwa DRC licha ya uwepo wa askari wa MONUSCO

Mkoa wa Kasai umekuwa ukishuhudia machafuko tangu Septemba mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 400 wameuawa katika machafuko na mapigano kati ya askari usalama na wanamgambo wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu, aliyeuliwa na maafisa usalama. 

Ijumaa iliyopita, Yvon Edoumou, afisa katika Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) alisema kuwa, asasi hiyo imesajili wakimbizi wa ndani milioni 1.09 katika mkoa wa Kasai, katikati mwa Kongo kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.

Aidha mauaji haya yanaripotiwa siku chache baada ya timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kugundua makaburi mengine 17 ya umati katika mkoa huo wa Kasai na kupelekea jumla ya makaburi ya umati yaliyogunduliwa hadi sasa na UN kufikia 40, katika eneo hilo ambalo lilishuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.

Miili iliyofukuliwa kutoka moja ya makaburi ya umati Kasai