Umoja wa Mataifa waitaka serikali ya Ethiopia kuwaachilia huru wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28660-umoja_wa_mataifa_waitaka_serikali_ya_ethiopia_kuwaachilia_huru_wapinzani
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Ethiopia kuwaachilia huru watu ambao walitiwa nguvuni katika maandamano dhidi ya serikali hiyo kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 05, 2017 04:04 UTC
  • Umoja wa Mataifa waitaka serikali ya Ethiopia kuwaachilia huru wapinzani

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Ethiopia kuwaachilia huru watu ambao walitiwa nguvuni katika maandamano dhidi ya serikali hiyo kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu.

Zeid bin Ra'ad, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa safari yake ya siku tatu ya kuitembelea Ethiopia ambapo ameitaka serikali ya Addis Ababa kuwaachilia huru wapinzani ambao walitiwa mbaroni katika maandamano ya kuipinga serikali ya nchi hiyo.

Wakati wa kujiri maandamano hayo

Katika maandamano ya kati ya mwaka jana 2016 na mwaka huu, wakati ambao serikali ya nchi hiyo ilikuwa imetangaza hali ya hatari nchini zaidi ya watu elfu 26 walitiwa mbaroni. Mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia alitupilia mbali pendekezo la kutaka kufanyika uchunguzi wa kujitegemea kuhusiana na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. Hivi karibuni pia, Ofisi ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia ilitoa ripoti inayosema kuwa, zaidi ya raia 669 waliuawa katika maandamano yaliyofanyika mwaka jana pekee dhidi ya serikali, katika mikoa ya Amhara na Oromia na maeneo mengine ya kusini mwa nchi hiyo.

Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia

Kadhalika mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema kuwa, makabila ya maeneo hayo ambayo yanaunda asilimia 60 ya jamii nzima ya Ethiopia yalikandamizwa vikali na askari usalama wakati wa maandamano na ghasia za mwaka jana zilizofanyika kupinga mfumo wa kisiasa na utawala wa sasa wa nchi hiyo ambao wanasema unawabagua.