May 06, 2017 04:12 UTC
  • Askari 3 wa Marekani wauawa na kujeruhiwa na al-Shabaab Somalia

Askari mmoja wa Marekani ameuawa kwa kufyatuliwa risasi katika operesheni ya pamoja ya US na jeshi la Somalia dhidi ya ngome ya wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab.

Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (Africom) imeripoti kuwa, mbali na mwanajeshi huyo kuuawa, wengine wawili wamejeruhiwa katika operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Barii, yapata maili 40 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.

Robyn Mack, Msemaji wa Africom ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wanajeshi hao wa Marekani wameuawa na kujeruhiwa katika operesheni iliyofanyika Mei 4.

Ramani ya Somalia

Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani aliidhinisha kutumwa makumi ya askari wa US nchini Somalia, idadi kubwa kuwahi kutumwa na US katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, tangu mwaka 1993.

Itakumbukwa kuwa, Marekani iliviondoa vikosi vyake nchini Somalia mwaka 1993, baada ya wanajeshi wake wasiopungua 18 kudhalilishwa kwa kuuawa na kisha miili yao kuburutwa ardhini katika mji mkuu Mogadishu.

Tags