May 17, 2017 07:33 UTC
  • Wimbi la wakimbizi wa CAR lamiminika nchini DRC

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusiana na wakimbizi ametangaza habari ya kumiminika maelfu ya wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika ripoti yake ya jana, kamishna huyo amesema, karibu wakimbizi elfu mbili na 750 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamemiminika katika mikoa ya Bas-Uele na Ubangi Kaskazini (Nord-Ubangi), huko kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakimbizi hao wamekimbia mapigano katika mji wa Bangassou wa kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na maeneo mengine ya mpakani.

Wanawake na watoto wadogo ndio wahanga wakuu wa machafuko

 

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na masuala ya wakimbizi  amesema, hali ya wakimbizi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo si nzuri hata kidogo.

Hivi sasa baadhi ya wakimbizi hao wamepewa makazi katika maeneo ya mashuleni, kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Maelfu ya raia wamekimbia makazi yao kutokana na kuongezeka mapigano ya kutumia silaha huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Tags