May 21, 2017 04:17 UTC
  • Mauaji yaendelea Afrika ya Kati, watu wengine 22 wauawa

Mapigano yameendelea kushuhudiwa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo watu 22 wameripotiwa kuuawa.

Diane Corner, naibu kamanda wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo amesema kuwa kwa akali watu 22 waliuawa katika mapigano ya wiki hii inayomalizika huko katika mji wa Bria, katikati mwa mkoa wa Haute-Kotto, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Corner amesema kuwa, miongoni mwa wahanga hao, 17 ni raia wa kawaida.

François Bozizé, rais wa zamani wa CAR

Aidha Diane Corner, naibu kamanda wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mjumbe maakumu wa Katibu Mkuu wa Umoja huo nchini humo amesisitiza juu ya udharura wa kusimamishwa mapigano baina ya makundi ya wabeba silaha ndani ya taifa hilo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano hayo katika mji wa Bria yamewalazimisha watu elfu 10 kuyahama makazi yao. Hayo yanajiri katika hali ambayo, mapema jana Umoja wa Mataifa ulilaani kitendo cha vyombo vya habari kupuuza kuakisi habari ya mashambulizi na mauaji ya makumi ya Waislamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Waislamu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaouawa kigaidi

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, karibu Waislamu 30 wameuawa hivi karibuni katika mji wa Bangassou kusini mashariki mwa nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya magenge yenye silaha, lakini vyombo vya habari kimataifa vimenyamaza kimya kana kwamba hakuna mauaji yoyote yaliyotokea. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia vitani mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani serikali ya wakati huo chini ya François Bozizé, rais wa zamani wa nchi hiyo.

Tags