Indhari juu ya kugeuka Afrika Kusini na kuwa nchi ya kimafia
Sambamba na kuendelea mivutano na malalamiko nchini Afrika Kusini, Makamu wa Rais wa nchi hiyo ametahadharisha kuhusiana na hatari ya kubadilika nchi hiyo kuwa ya Kimafia.
Cyril Ramaphosa Makamu wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini sanjari na kumkosoa rais huyo amesisitiza kuwa, kama chama tawala wa ANC kinataka kisipoteze himaya na udhibiti wa jamii ya nchi hiyo, basi hakipaswi kuruhusu Afrika Kusini igeuke na kuwa nchi ya kimafia. Ramaphosa ametoa wito wa kuweko uchunguzi huru kuhusiana na mafaili ya ufisadi ambayo yanawatilia alama ya swali baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo.
Cyril Ramaphosa ametoa matamshi hayo katika hali ambayo, chama tawala cha ANC Disemba mwaka huu kinatarajiwa kumtangaza mrithi wa Rais Jacob Zuma ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kufanyika mwaka 2019. Ramaphosa anatajwa kuwa mgombea mkuu katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa chama wa kumteua mgombea wake.
Kwa muda sasa utendaji wa Rais Jacob Zuma umekuwa ukiandamwa na wimbi la ukosoaji wa vyama mbalimbali vya upinzani vya nchi hiyo. Tangu Rais Zuma alipoingia madarakani mwaka 2009 amekuwa akikabiliwa na mafaili mbalimbali ya ufisadi wa kifedha. Hata kama daima Rais Zuma amekuwa ni mwenye kukana tuhuma dhidi yake na wakati mwingine hata kuahidi kuwachukulia hatua wahalifu katika uwanja huo, lakini wanaharakati wa masuala ya kisiasa nchini Afrika Kusini na akthari ya vyama vya kisiasa vya nchi hiyo vimekuwa vikimtaka kiongozi huyo ajiuzulu na kuachia ngazi kabla ya kumalizika kipindi chake cha uongozi.
Baada ya hivi karibuni kushika kasi malalamiko, Rais Zuma akiwa na lengo la kupunguza joto la upinzani huo alimfuta kazi Waziri wa Fedha Pravin Gordhan. Hata hivyo kinyume na matarajio yake, hatua hiyo ilichochea zaidi moto wa upinzani dhidi yake. Rais wa Afrika Kusini alitaja sababu ya kumfuta kazi waziri huyo kwamba, ni katika juhudi za kupambana na ufisadi. Hata hivyo wapinzani wanapinga hilo na kusisitiza kwamba, Pravin Gordhan alifutwa kazi kwa sababu za kisiasa kutokana na waziri huyo kufichua upokeaji rushwa wa Rais Zuma.
Malalamiko hayo ya kisiasa nchini Afrika yanaendelea kushuhudiwa katika hali ambayo, nchi hiyo inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Hata kama siku zote Afrika Kusini imekuwa ikihesabiwa kuwa na ukuaji mzuri wa kiuchumi , lakini hivi sasa uchumi wa nchi hiyo umo katika hali ya kuzorota na kuporomoka. Asilimia 25 ya kiwango cha ukosefu wa ajira, kuongezeka gharama za maisha, kuporomoka thamani ya Rand ambayo ndiyo sarafu ya nchi hiyo na ukame ulioyakumba baadhi ya maeneo ya nchi ni mambo ambayo yametoa pigo kubwa kwa uchumi wa Afrika Kusini. Suala hilo limepelekea kupungua kiwango cha uzalishaji na kupanda kwa ukosefu wa kazi hususan kwa wakulima.
Hivi karibuni msemaji wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Madini nchini Afrika Kusini alitangaza kuwa, sekta ya madini nchini humo nayo, kwa sasa inakabiliwa na mgogoro wa ukosefu wa ajira na kuna uwezekano wa kufutwa zaidi ya nafasi 36,000 za ajira.
Kupungua ukuaji wa uchumi nchini Afrika Kusini kumepelekea kutokea mivutano ya kijamii. Katika hali ambayo, akthari ya fursa za kazi zimo mikononi mwa raia wa kigeni, hali ya sasa ya kiuchumi imewafanya raia wa nchi hiyo wanaotafuta kazi kuamiliana vibaya na wafanyakazi wa kigeni wakiwaona kama chanzo cha hali wanayokabiliwa nayo.
Majimui ya mambo hayo, imeifanya nafasi ya chama tawala cha ANC kuwa hatarini. Mfano wa hilo ni kushindwa vibaya chama hicho katika uchaguzi wa Mabaraza ya Miji wa mwaka jana.
Hata kama imepita miezi kadhaa tangu kufanyika kwa uchaguzi huo, lakini wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushindwa huko ni ishara ya kudhoofika nafasi ya chama cha ANC katika fikra za waliowengi nchini humo hususan miongoni mwa wazalendo.
Hivi sasa utendaji mbaya wa Rais Zuma na tuhuma za ufisadi anazokabiliwa nazo, ni mambo ambayo yanatathminiwa na wachambuzi wa mambo kwamba, yamechangia kupungua himaya na uungaji mkono pamoja na mapenzi ya wananchi kwa chama hicho.
Ni kwa kuzingatia hayo, ndio maana kundi ndani ya chama cha ANC likamtaka Zuma ajiuzulu. Kundi hilo linahofia kurejea udikteta nchi humo na kupungua siku baada ya siku mapenzi ya watu kwa chama hicho.