May 29, 2017 04:01 UTC
  • Misri: Kuna uwezekano tukashambuliwa tena na magaidi

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema kuwa, kuna uwezekano makundi ya kigaidi yakafanya tena mashambulizi nchini humo, hivyo imevitaka vikosi vya usalama kuchukua hatua kali za kiusalama kukabiliana na jambo hilo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema hayo leo Jumatatu katika taarifa yake maalumu na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa taarifa maalumu za kiintelijensia, magaidi wamepanga kufanya mashambulizi mengine katika makanisa na maeneo ya kidini ya Wakristo nchini Misri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, picha za watu wanaodhaniwa huenda wakafanya mashambulizi hayo ya kigaidi zimetumwa katika vituo vya usalama na kijeshi kote nchini Misri.

Hata hivyo taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri haikusema ni maeneo gani hasa mashambulizi hayo yanadhaniwa yatatokea.

 

Taarifa hiyo imetolewa baada ya watu wenye silaha kushambulia mabasi yaliyokuwa na Wakristo kusini mwa mji mkuu Cairo siku ya Ijumaa na kuua watu 28 na kujeruhi makumi ya wengine. Genge la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na shambulio hilo.

Baada ya shambulizi hilo, ndege za kivita za Misri siku za Ijumaa na Jumamosi zilifanya mashambulizi katika eneo la Dernah la nchini Libya. Misri inaamini kuwa mashambulizi dhidi ya Wakristo wa nchi hiyo yalifanywa na watu waliopata mafunzo ya kigaidi katika eneo la Dernah nchini Libya.

Jeshi la Libya lililoko chini ya Jenerali Khalifa Haftar lilisema kuwa, lilishirikiana na Misri katika mashambulizi hayo.

Tags