Chama tawala Afrika Kusini chatangaza kumuunga mkono Rais Jacob Zuma
Chama cha Kongresi ya Taifa ANC kinachotawala nchini Afrika Kusini kimetangaza kuwa, tume tendaji ya chama hicho inamuunga mkono Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.
Jumatatu ya jana chama hicho kilitoa taarifa ambayo ilipinga pendekezo la baadhi ya viongozi la kumtaka Rais Zuma ang'atuke madarakani na kukiondoa chama hicho katika ulingo wa utawala. Vyombo mbalimbali vya habari vimetangaza kuwa, Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashinikizo mengi ndani ya chama Jumapili iliyopita aliponea chupuchupu kutokana na kupigiwa kura na kamati tendaji ya chama tawala cha ANC ya kutokuwa na imani naye.
Katibu Mkuu wa chama cha Kongresi ya Taifa nchini humo amewambia waandishi wa habari kwamba, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wamemtaka Rais Zuma kuachia madaraka. Gwede Mantashe ameongeza kuwa, wale wote wanaomtaka Rais Zuma kuondoka madarakani, hawakusudii kusambaratisha shakhsia ya rais huyo tu, bali wanakusudia pia kukiondoa madarakani chama hicho tawala. Imepangwa rais huyo kuachia ngazi ya uenyekiti wa chama tawala ifikapo mwezi Disemba mwaka huu, huku uongozi wake wa urais ukimalizika mwaka 2019.